Ad Code

MUNGU NDIYE ATENDAYE MIUJIZA


 

unaweza kuona ya kwamba vitu vyote ambavyo Mungu ameviumba ni muujiza kwetu. Pia aliumba kwa namna ya pekee jua, mwezi, nyota na sayari nyingine mbalimbali ambazo  aliziweka juu ya anga, huku zikiwa zinaning’inia bila kushikiliwa na kitu chochote, wala hazidondoki. Pia bahari nayo imekaa mahali ilipoamriwa bila kuvuka mpaka alioiwekea Bwana. Kwa hiyo tunapoona uumbaji wa vitu vyote ambavyo Mungu aliviumba vinashangaza, navyo ni ishara  kwetu ya kutosha na kutambua ya kwamba Mungu yupo. Kwa sababu hiyo yatupasa kufahamu ya kwamba yeye ndiye mwenye uwezo wote, yeye hutenda mambo yote sawasawa na mapenzi yake. Kwa hiyo tunaweza kuona Sababu ya Mungu kufanya muujiza kwa mkono wa Musa mbele ya Farao na Wamisri. Mungu akamwambia Farao; “lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote.” Kutoka 9:16. Kutokana na andiko hili hapa juu linazungumzia Mungu alifanya miujiza ili kumwonyesha Farao uweza wake. Na Kusudi lingine ni ili jina la Mungu litangazwe duniani kote. Ndio maana hata sasa Jina la Mungu linatangazwa ulimwengu kutokana na matendo makuu aliyoyatenda kwa nyakati tofauti.

Pia yatupasa kutambua ya kwamba Mungu ndiye atendaye miujiza yote. Kwa sababu hiyo hakuna mtu mwenye uwezo wa kufanya muujiza. Ndio maana mtume petro aliwahutubia Waisraeli akawaambia; “Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya: Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua;” Matendo ya Mitume 2:22. Hili andiko hapa juu linamaanisha ya kwamba Mungu alifanya miujiza, ajabu na ishara kwa mkono wa Yesu Kristo. Kwa hiyo Mungu alimtumia kufanya matendo ya miujiza.

Kwa sababu hiyo yawapasa waliookoka kuwa makini na kufahamu kuna kanuni na mwongozo wa neno la Mungu kuhusu kufanya muujiza. Katika kanisa kuna baadhi ya wakristo  ambao wamejaliwa kuwa na karama ya muujiza. Wanaweza kutumiwa na Mungu ikiwa watafuata kanuni na mwongozo wa neno la Mungu linavyosema. Kwa hiyo mtu anaweza kufanya muujiza kwa mapenzi ya Mungu na kuongozwa na Roho wa Mungu. Kwa sababu hiyo mtu hawezi kufanya muujiza kwa matakwa yake au kama yeye apendavyo. Lakini kama mtu atataka kufanya muujiza  kwa matakwa yake haiwezi kutokea. Ila kwa mtu aliye mnyenyekevu na kutaka mapenzi ya Mungu yatimizwe, huyo ndiye hutenda miujiza kwa imani na kuongozwa na Roho Mtakatifu.





Chapisha Maoni

0 Maoni

Close Menu